Mahakama ya Rufaa nchini Kenya imependekeza Sheria ya Unyanyasaji wa Kingono kufanyiwa mabadiliko na kupunguza umri wa kushiriki ngono kuwa miaka 16 badala ya 18.
Jopo la Majaji watatu, Nambuye, Daniel Musinga na Patrick limetoa mapendekezo hayo Ijumaa, Machi 22 walipokuwa wakitoa uamuzi wa rufaa kuhusu kifungo cha miaka 15 jela dhidi ya kijana ambaye alimpa ujauzito msichana mwenye umri wa miaka 17.
Kwa mujibu wa majaji hao, nchi hiyo inapaswa kujadili kwa kina na kutafakari mabadiliko ya ukuaji, ulinzi wa watoto na adhabu kwa watu wanaoshiriki ngono na watoto wenye umri wa miaka 16 na 17.
Wameeleza kuwa watu wengi wanafungwa miaka mingi jela kwa kosa la kufanya ngono na watu wenye umri kati ya miaka hiyo ambao huwa wameridhia na pia wana muonekano kama wa watu wazima.
“Jela zetu zinajazwa na vijana wadogo ambao wanatumikia vifungo virefu kwa kufanya mapenzi na wasichana wadogo ambao kukubali kwao kunatafsiriwa kisheria kuwa sio hoja ya utetezi kwa sababu walikuwa chini ya umri wa miaka 18,” Majaji wameeleza.
Kwa mujibu wa jopo la majaji hao, sio uhalisia kufikiri kuwa watu wazima na watoto wenye miaka kati ya 16 na 17 hawafanyi mapenzi.
“Wanaweza kuwa hawajafikia umri wa utu uzima lakini wanaweza kuwa wamefikia umri wa kujitambua na kufanya maamuzi kuhusu maisha yao na miili yao. Huo ni mchakato wa ukuaji,” wameeleza.
Katika kesi husika, kijana Eliud Waweru alikuwa amefungwa jela miaka 15 kwa kosa la kumpa ujauzito msichana ambaye alikuwa amemaliza kidato cha nne lakini ana umri wa miaka 17.
Ilibainika kuwa Waweru alikuwa amekubaliana na baba wa mtoto huyo kulipia mahari ya Sh80,000 za Kenya, mbele ya kiongozi wa eneo walilokuwa wakiishi.
Ilielezwa kuwa baada ya Waweru kushindwa kulipia kiasi hicho cha fedha licha ya kumpa ujauzito msichana huyo, alifunguliwa kesi mahakamani na kutupwa jela, miaka nane iliyopita.
Jopo hilo la Majaji lilimuachia huru Ijumaa iliyopita baada ya kutumikia kifungo hicho kilichotolewa awali na Mahakama Kuu.