leo Jumanne Mei 7, 2019 Jaji Stephen Magoiga wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ameamuru mali za kampuni ya upatu ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), zitaifishwe.
Jaji Magoiga ametoa uamuzi huo wa kutaifishwa kwa mali hizo za kampuni ya DECI (maarufu kupanda mbegu na kuvuna) zikiwemo pesa taslimu Sh14.1 bilioni, zilizoko katika akaunti za benki mbalimbali jijini Dar es Salaam pamoja na majumba na viwanja katika mikoa mbalimbali na magari ya kifahari umetolewa .
Uamuzi huo ni baada ya kukubaliana na hoja za maombi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwa mali hizo zilitokana na mapato ya uhalifu yaani kuendesha shughuli za upatu na kukusanya pesa kutoka kwa umma bila kuwa na leseni.
Jaji Magoiga amesema ameridhika na hoja na ushahidi wa DPP baada ya wakurugenzi wa Deci kushindwa kutoa ushahidi wa jinsi walivyozipata mali hizo, licha ya kupinga tu kwa maneno kwamba hazikutokana na Deci.
Jaji Magoiga amefafanua viongozi hao wa Deci kwa kushindwa kutoa ushahidi wa kupinga mali hizo kutaifishwa wameshindwa kutimiza wajibu wao na matakwa ya kisheria kwa mujibu wa Sheria ya kushulikia mali zinazotokana na Uhalifu (POCA).
“DPP au Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) anapowasilisha mahakamani maombi ya kutaifishwa kwa za washtakiwa waliotiwa hatiani kwa uhalifu, mtu anayepinga maombi hayo anapaswa kuwasilisha mahakamani ushahidi kuwa mali hizo hazikutoakana na uhalifu.”
DPP alifungua maombi hayo Machi, 2019, miaka takribani sita baada viongozi hao wa DECI kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya jinai namba 109 ya mwaka 2009, kwa kosa la kuendesha biashara ya upatu kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kutoka Mwananchi, viongozi wa DECI, ambao walikuwa wachungaji, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kipentekosti, walitiwa hatiani kwa kosa hilo mwaka 2013 na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya jumla ya Sh21 milioni. Walilipa faini hiyo na hivyo wakaepuka kifungo.
Waliotiwa hatiani katika kesi hiyo, ambao ndio wajibu maombi katika maombi ya DPP ni Jackson Sifael Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saigaran ole Loitginye na Samwel Sifael Mtares.
Aidha, wakili wa wajibu maombi hayo, Majura Magafu aliiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo akidai kuwa mwombaji ameshindwa kutoa ushahidi mahakamani kuthibitisha kuwa mali hizo zote zimetokana na makosa hayo yaliyowatia hatiani.