Mahakama ya Rufaa ya Tanzania imeipitisha adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela na faini ya Sh. 85,980,000, dhidi ya kigogo wa dawa za kulevya, Abdallah Rajabu Mwalimu, aliyekutwa na hatia ya kusafirisha kete 54 za dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa gramu 716.5.
Jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa, Batuel Mmilla, Ferdinand Wambali na Mary Revina wote walitoa uamuzi uliomtia hatiani Mwalimu, wakitupilia mbali malalamiko yake dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu.
“Kwa kuzingatia rufaa iliyowasilishwa na mlalamikaji, tumebaini kuwa maombi na sababu zake hazina mashiko, hivyo tunayatupilia mbali,” Mahakama imeeleza.
Mahakama pia imeeleza kuwa imejihakikishia mwendesha mashtaka amethibitisha pasipo na shaka sababu za kumtia hatiani Mwalimu kwa makosa hayo.
“Tumeridhishwa na uamuzi wa Mahakama, kwakuwa mahakama imefanya tathmini ya kutosha ya vielelezo vyote vilivyowasilishwa na pande mbili na mwisho wamefikia uamuzi sahihi kwamba mlalamikaji hakufanikiwa kuthibitisha pasipo na shaka madai ya kutotendewa haki,” wanasheria wa Serikali, Elizabeth Mkude, Batilda Mushi na Candid Masua wameeleza.
Mwalimu alikamatwa Februari 4, 2011 majira ya saa saba na nusu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alipokuwa anafanya utaratibu wa kusafiri kwenda nchini Afrika Kusini. Alikutwa na kete 54 za dawa hizo za kulevya.