Mahakama ya Hakimiu Mkazi Mkoa wa Kigoma imefuta kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo dhidi ya aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila baada ya upande wa serikali kushindwa kupeleka mashahidi kwa kipindi kirefu.

Katika kesi hiyo, Kafulila alikuwa anashtakiwa kwa kosa la kumtolea lugha ya matusi Mkuu wa Wilaya hiyo, Khadija Nyembo alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara wilayani humo, Agosti 1 mwaka 2013.

Akitoa uamuzi juu ya kesi hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Silvester Kainda alieleza kuwa ameamua kuifuta kesi hiyo kwa kuwa ni kesi ya muda mrefu na upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha mashahidi huku wakiomba kupewa muda kila inaposomwa.

Katika mashtaka hayo, wakili wa serikali Shabani Masanja alieleza mahakamani hapo awali kuwa Kafulila alimtolea lugha chafu mkuu huyo wa Wilaya huku akinukuu matamshi ya yake, “Mtu kama Hadija Nyembo unamuokota wapi na kumpa ukuu wa wilaya, unamchukua shangingi la mjini uko unasema aliwahi kuwa mkuu wa wilaya, mkuu wa wilaya akija hapa maana yake polisi wa wampigie saluti, kuna polisi wenye akili hapa kuliko huyu mkuu wa wilaya, wanampigia saluti basi tu manake hana akili.”

Kafulila alikuwa amekanusha tuhuma hizo huku upande wa serikali ukitakiwa kuwasilisha ushahidi ambao ulikwamba kwa zaidi ya siku 60 na kupelekea kesi hiyo kufutwa.

 

Siri: Kalamu zenye Kamera zilivyowezesha ushindi wa Ukawa Umeya Kinondoni na Ilala
Walimu wapigwa marufuku kupaka lipstick, wanja

Comments

comments