Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu mmiliki wa Kampuni ya kufua umeme ya IPTL, Harbinder Seth kulipa fidia ya Shilingi Billioni 26 za Kitanzania.

Uamuzi huo umetolewa  leo Juni 16,2021 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ya Uhujumu uchumi namba 27/2017 ilipoitwa mahakamani hapo kwa makubaliano na Seth kupatikana na hatia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Hakimu Huruma Shaidi amesema “Ni dhahiri umekaa mahabusu kwa muda mrefu takribani miaka minne ni muda mwingi wa kutosha na ni wazi umeona mengi na kujifunza mengi ukiwa gerezani.”

“Pia kwa mantiki hiyo Mahakama inaamua kukupa onyo usije ukatenda makosa tena na utakuwa chini ya uangalizi kwa muda wa mwaka mmoja hayo ndio maamuzi ya Mahakama, kuhusu nyaraka mbalimbali ikiwemo Passport ya kusafiria arudishiwe,” amesema Hakimu Huruma Shaidi.

Seth aliandika barua hiyo Juni 10, kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akiomba kukiri mashtaka yake na kupunguziwa adhabu.

Seth ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), amepewa masharti ya kutotakiwa kutenda kosa lolote kwa kipindi cha mwaka kuanzia leo Juni 16, 2021.

Seth amekubali kuweka hati ya kiwanda cha kufua umeme cha IPTL chenye namba 45566, kiwanja namba 292/2 kilichopo Kunduchi salasala kama dhamana iwapo atashindwa kulipa fedha hizo.

 Mshtakiwa Seth amesomewa upya mashtaka yake ambapo sasa ameshtakiwa na kosa moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuondolewa mashtaka mengine 11 ambayo yalikuwa yakimkabili yeye na mshtakiwa mwenzake James Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi mwenza wa IPTL amabye yeye bado anasota rumande.

Katika shtaka hilo jipya inadaiwa katika tarehe tofauti tofauti kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 2014 huko katika benki ya Stanbic Tawi la Kinondoni na benki ya biashara ya Mkombozi Tawi la St. Joseph ndani ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam mshtakiwa alitenda kosa.

RC Makalla azitaka Halmashauri kujiepusha na hati chafu
Tulitakiwa tuwe na kina Diamond 10 watakao ingia tuzo za BET