Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo imemuachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Habari Tanzania (TBC), Tido Mhando baada ya kutomkuta na hatia.
Tido alikuwa akikabiliwa na mashtaka matano, manne ya kutumia vibaya madaraka na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh. 887.1 milioni kupitia mikataba miwili aliyoisaini na makampuni ya Startimes na Channel 2 Group Cooperation akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC kwa lengo la kuingia ubia na makampuni hayo katika kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda mfumo wa dijitali.
Upande wa Mashtaka uliiambia Mahakama kuwa akiwa Dubai, Oktoba 30 mwaka jana mshtakiwa alisaini mkataba kati ya TBC na kampuni ya Channel 2 bila kuzingatia sheria ya manunuzi ya umma. Ilielezwa kuwa katika siku hiyo, aliisababishia Serikali hasara ya Sh. 887.1 milioni.
Akisoma hukumu ya kesi dhidi ya Tido, Hakimu Mkuu, Huruma Shaidi amesema kuwa mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kutosha usioacha shaka.
Sehemu ya utetezi wa Tido aliouwasilisha mahakamani wakati wa mchakato wa kujitetea, alieleza kuwa mkataba aliouingia kati yake na Startimes uliidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa TBC, hivyo yeye aliagizwa kuusaini.
Alisema mkataba aliousaini peke yake na Channel 2 ulikuwa mkataba wa makubaliano ya awali na sio mkataba wa mradi kamili. Alifafanua kuwa mkataba kamili ni ule wa kati ya Startimes na TBC ambao aliusaini yeye pamoja na mwanasheria wa TBC kama inavyoelekezwa na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Januari 26 mwaka jana. Hivyo, imehitimishwa baada ya mwaka mmoja kamili.