Naibu Msajili wa Mahakama Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Projest Kahyoza ameahirisha amuzi wa kesi ya kupinga mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, unaohusu uwekezaji katika Bandari za Baharini na Maziwa nchini, uliokuwa umepangwa kutolewa hii leo Agosti 7, 2023.
Akiahirisha uamuzi huo, Naibu Msajili Kahyoza amesema, “ulikuwa umepangwa kutolewa leo, kwa bahati mbaya mwenyekiti wa jopo amepata dharura kwa hiyo wamekubaliana kwamba mpaka wote wawepo hivyo ameelekeza maamuzi haya yasomwe Alhamisi ya wiki hii, tarehe 10, 2023.”
Kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 ilifunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na Mawakili wanne kutoka mikoa tofauto dhidi ya Serikali akiwemo Frank Nyalus, Alphonce Lusako, Raphael Ngonde, na Emmanuel Chengula.
Wanasheria hao waliofungua kesi, wanapinga makubaliano hayo masharti ya baadhi ya ibara zake yanakiuka Sheria za Nchi za Ulinzi wa Rasilimali na Maliasili za na Katiba ya Nchi, yanahatarisha mamlaka na usalama wa Taifa na yaliridhiwa na Bunge kinyume cha utaratibu.