Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam, leo imetoa uamuzi kuhusu ombi la upande wa mashtaka la kutoa hati ya kumkamata Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kwa kutoonekana mahakamani bila kuwasilisha maendeleo ya matibabu yake.
Upande wa Mashtaka uliiomba Mahakama kutoa hati hiyo kwa maelezo kuwa mshtakiwa anaonekana akiendelea kutoa mihadhara sehemu mbalimbali duniani wakati hafiki mahakamani hapo.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amelikataa ombi hilo na kuwaonya wadhamini wa Lissu ambao walifika mahakamani hapo kutoa sababu za mshtakiwa kutofika mahakamani pamoja na hali ya afya yake kama walivyotakiwa.
“Hati ya kumkamata mshtakiwa kwa sasa haiwezi kutolewa,” alisema Hakimu Simba. “Hivyo, nawaonya washtakiwa kuhakikisha wanafika mahakamani kila kesi hii inapotajwa,” aliongeza.
Awali, wadhamini hao waliieleza mahakama kuwa Lissu hakufika mahakamani hapo kwakuwa anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji.
Mmoja wa wadhamini hao alisema kuwa hakuwa anafika mahakamani hapo kwakuwa mzazi wake anaumwa na amelazwa.
Mdhamini wa pili yeye aliomba radhi kwa kutofika akieleza kuwa hakuwa anajua kama alitakiwa kufika mahakamani hapo kila kesi inapotajwa.
Lissu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya uchochezi. Wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha kwenye gazeti la Mawio taarifa yenye kichwa cha habari, “Machafuko yaja Zanzibar.” Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Wahariri wa Gazeti hilo, Simon Mkina na Jabir Idrisa pamoja na Mchapaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.