Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa hati ya kuwaita mahakamani wadhamini wa Makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA , Tanzania Bara,Tundu Lissu, kufika mahakamani hapo Januari 25, 2021 bila kukosa.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa hati ya kuwaita mahakamani wadhamini wa Makamu mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara,Tundu Lissu, kufika mahakamani hapo Januari 25, 2021 bila kukosa.
Wadhamini hao wanatakiwa kufika mahakamani hapo ili wajieleze sababu za kushindwa kufika mahakamani huku wakishindwa kumpeleka Lissu mahakamani hapo kama sheria inavyowataka.
Hatua hiyo imekuja baada ya mshtakiwa huyo pamoja na wadhamini wake kushindwa kufika mahakamani hapo kusikiliza kesi yake ya jinai namba 233/2016 iliyopo mahakamani hapo.
Hii ni mara ya tano, kwa Lissu kushindwa kufika mahakamani hapo kuhudhuria kesi zake, tangu aliporejea nchini Julai 29,2020, akitokea nchini Ubeljiji alipokuwa anapatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajafahamika.
Jana, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, aliieleza Mahakama hiyo mbele ye Hakimu Mwandamizi, Rashid Chaungu kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya uamuzi kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la, lakini mshtakiwa na mawakili wake hawakuwapo mahakamani.
“Kutokana na mshtakiwa pamoja na wadhamini wake kushindwa kufika mahakamani hapa bila taarifa, tunaomba mahakama itoe hati ya kuwaita wadhamini wa Lissu wafike mahakamani hapa ili kesi yake iweze kuendelea, kwa sababu imeshindwa kuendelea kwa muda mrefu sasa” alidai wakili Simon.
Hakimu Chaungu, baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, alikubaliana na ombi hilo na kutoa hati ya kuwaita wadhamini wa Lissu wafike mahakamani hapo Januari 25, 2021 itakapotajwa.
Tayari upande wa mashtaka umeshafunga ushahidi wao tangu Septemba 4, 2017, na kwamba kesi iyo ilitakiwa kutolewa uamuzi Oktoba 4, 2017 kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.
Hata hivyo, uamuzi huo ulishindwa kutolewa baada ya mshtakiwa huyo kushambuliwa kwa risasi na watu ambao bado hawajafahamika na hivyo kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la kutoa maneno ya uchochezi katika kesi ya jinai 233/2016. Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo, Juni 28, 2016 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mpaka sasa Lissu anakabiliwa na kesi tano za uchochezi, zilizopo kwa mahakimu tofauti, katika Mahakama hiyo.