Watu wawili, Saidi Hussein (38), mkazi wa Kilimahewa na Leonard Stephano (37), wa Ibungilo wote wa Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilayani humo na kusomewa shtaka lenye makosa sita ikiwemo la kuuza Petroli na Dizeli bila leseni.
Washtakiwa hao katika kesi ya jinai namba 146/2023 wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na Kifungu namba 131 (1), (4) cha Sheria ya Petroli toleo namba 21 ya mwaka 2015 na kukutwa na mali zinazosadikika kuwa ni za wizi kinyume na Kifungu namba 312 (1) (b) cha sheria ya petroli toleo namba 21 ya mwaka 2015.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Fortunatus Kabaja Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mwanahawa Changale alisema washtakiwa walitenda makosa hayo Septemba 23, 2023, eneo la Bwiru Wilaya Ilemela Mkoani Mwanza.
Amesema, “Washtakiwa walikamatwa na maofisa wa polisi wakiwa na lita 5 za mafuta ya petroli, lita 235 za mafuta ya petroli na mipira 23 ya plastiki vyote vikiwa na thamani zaidi ya shilingi milioni moja na laki tisa kinyume na sheria.”
Aidha ameongeza kuwa, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kinyume na Kifungu namba 131 (1), (4) cha Sheria ya Dizeli toleo namba 21 ya mwaka 2015 na kutunza petroli kinyume na sheria kifungu namba 178 (1), (3) cha sheria ya Petroli ya mwaka 2015, toleo namba 21.
Makosa mengine ni kuuza mafuta ya Petroli bila kuwa na vifaa vya kiusalama kinyume na Kifungu namba 179 (1), (2) (b) ya Sheria ya Petroli toleo namba 21 ya mwaka 2015, Kuuza vifaa vya petroli kinyume na sheria kifungu namba 179 (1), (2) (c) ya sheria ya Petroli toleo namba 21 ya mwaka 2015.
Baada ya kusomewa mashtaka, walishindwa kukidhi masharti vya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili ambai ni watumishi wa Serikali kwa kila mmoja, barua ya utambulisho na kusaini bondi ya dhamana yenye thamani ya milioni kumi na hivyo kurejeshwa rumande na shauri hilo liliahirishwa hadi Oktoba 4, 2023.