Tume ya haki za binadamu na utawala bora (THBUB) imetakiwa kusimamia misingi ya utendaji wake wa kazi na kuimarisha utawala bora ili kuboresha utoaji wa huduma za serikali kwa wananchi.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma Novemba 18, 2019 na Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Augustino Mahiga katika kikao chake na Mwenyekiti wa Tume ya haki za binadamu na utawala bora Mathew Mwaimu kilichofanyika kwenye ofisi za wizara ya katiba na sheria.
Amesema tume hiyo ni chombo muhimu ambacho kimepewa mamlaka ya kusimamia mambo mawili ambayo ni haki za binadamu na utawala bora na hivyo kwa kuimarisha utendaji wake ikiwemo kusimamia utawala ni wazi kuwa jamii itapata huduma za Serikali kwa ufasaha.
“Tume hii katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yake imekuwa ikifanya kazi kubwa katika masuala ya haki za binadamu zaidi ya utawala bora sasa katika awamu hii ya tano mueLekeze nguvu zaidi katika kuimarisha misingi ya utawala bora,” amebainisha Waziri Mahiga.
Aidha katika hatua nyingine Waziri Mahiga ameitaka tume kutoa elimu kwa jamii juu ya namna haki za binadamu zinavyotekelezwa licha ya uwepo wa changamoto zinazoainishwa na wadau wa masuala ya haki za binadamu ambazo serikali ya awamu ya tano imekuwa ikizifanyia kazi kwa vitendo.
Waziri Mahiga ametaja baadhi ya mambo ambayo yanafanywa kwa vitendo na Serikali ya awamu ya tano kuwa ni pamoja kutoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi sekondari, huduma za afya kwa wazee wanaopata matibabu bure, na upatikanaji wa bima ya afya kwa wananchi.
“Jitihada zote hizi za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwapatia huduma wananchi hazijaelezwa vya kutosha na wahusika sasa tume tumieni nafasi yenu kuyaeleza haya kwa jamii ili iweze kuelewa kwa ufasaha” amesisitiza Waziri Mahiga.
Awali Katibu mkuu wizara ya katiba na sheria Prf. Sifuni Mchome amemueleza mwenyekiti wa tume kuwa masuala ya haki za binadamu yanafanywa na taasisi nyingi na hivyo kipindi hiki wawekeze nguvu zao katika kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria nchini.
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu na utawala bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amesema dhamana waliyopewa wataitumia vyema katika kusaidia serikali kutimiza malengo yake ya kuifikisha nchi katika uchumi wa kati kwa kuimarisha utawala bora.
Katika ziara hiyo Jaji mstaafu Mwaimu aliongozana na Makamu mwenyekiti Mohamed Khamis Hamad na makamishna watano ambao ni Dkt. Fatma Rashid Khalfan, Thomas Masanja, Amina Talib Ali, Khatib Mwinyi Chande na Nyanda Josiah Shuli.