Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Algeria na Klabu ya Manchester City, Riyad Mahrez ameripotiwa kukubali ofa matata ya Pauni 410,000 kwa juma, ili akakipige Saudi Arabia.
Lakini, Mahrez hatalazimisha uhamisho wa kuachana na Man City baada ya kubeba mataji matatu msimu uliopita chini ya Kocha Pep Guardiola.
Mahrez mwenye umri wa miaka 32, amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Man City tangu aliposajiliwa kwa uhamisho wa Pauni 60 milioni akitokea Leicester City mwaka 2018.
Staa huyo alifunga mabao 78 katika mechi 236 alizochezea Man City, akishinda mataji manne likiwamo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lakini, Mahrez kwa sasa anatajwa kama mmoja wa mastaa wenye majina makubwa anayeweza kuhamia Saudi Arabia.
Al-Ahli imemsajili Mlinda Lango wa Chelsea, Edouard Mendy na imetoa pesa za kutosha kumchukua Roberto Firmino.
Na ripoti zinafichua kwamba ni hao hao Al-Ahli wanaomtaka Mahrez na kumwekea mezani ofa ya mshahara wa Pauni 410,000 kwa juma, na mchezaji huyo yupo tayari kwenda kukipiga huko Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, hatima yake ipo kwenye mikono ya Man City, ambapo Kocha Guardiola ameripotiwa hana mpango wa kumwachia aondoke.
Staa mwanzake, Bernardo Silva naye amekumbana na ushawishi mkubwa wa kifedha kutoka kwa timu za Saudi Arabia.