Baraza Kuu la Waislamu Tanzania BAKWATA limesema mahujaji waliochanjwa chanjo ya Uviko-19 mwaka mmoja au miaka miwili iliyopita hawataruhusiwa kwenda Hijja hadi watakaporudia kuchanja chanjo hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Juni 25,2022 na Mkurugenzi wa Hija wa BAKWATA, Haidary Kambwili, kwenye semina ya mahujaji iliyofanyika ofisi za Makao Makuu ya BAKWATA jijini Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya mahujaji hao kwenda nchini Saudi Arabia kuhiji.
Kambwili amesema miongoni mwa masharti makuu wanayopaswa kuyafuata wanaotaka kwenda hijja ni kuchanja saa 72 kabla ya kuanza safari.
Kambwili amesema utaratibu huo umetolewa na nchi ya Saud Arabia ikiwa ni mkakati endelevu wa nchi hiyo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.
Kuhiji katika mji Makka uliopo nchini Saudi Arabia ni moja kati ya nguzo tano za uislamu na nguzo hii hufanywa na yule amabe ana uwezo wa kufika na kuhudhuria Hijja na kurudi bila kuwa na deni lolote.