Urari wa kibiashara kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Saudia Arabia umezidi kukua ambapo mpaka sasa miradi 14 ya uwekezaji kutoka nchini humo imesajiliwa katika kituo cha taifa cha uwekezaji (TIC), huku kampuni nane za kitanzania zikipata kibali cha kuuza minofu ya samaki nchini humo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Balozi wa Saudi Arabia anayemaliza muda wake wa uwakilishi nchini, Mohamed Bin Mansour Al Maliki.
“Kwa hakika kipindi hiki mahusiano ya Saudi Arabia na Tanzania yameimarika vizuri kwa manufaa ya pande zote mbili, ambapo katika sekta ya uwekezaji kumekuwa na miradi 14 iliyoandikishwa katika Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC), ambapo uwiano wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Saudi Arabia unazidi kuongezeka na kuimarika,” amesema Balozi Ibuge.
Balozi Ibuge ameongeza kuwa zipo fursa nyingi za uwekezaji ambapo kupitia juhudi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo, kampuni kubwa ya Serikali ya Saudi Arabia ipo katika hatua za mwisho za kuja kuwekeza katika sekta za mifugo na kilimo hapa nchini.
Aidha, Balozi Ibuge ameeleza kuwa kwa upande wa Tanzania kampuni nane zimepata kibali cha kuuza minofu ya samaki katika soko la Saudi Arabia, ikiwa ni moja kati ya juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Balozi Al Maliki kwa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mahusiano ya nchi zote mbili.
Kwa upande wake Balozi, anayemaliza muda wake wa uwakilishi nchini, Al Maliki ambaye amekuwa nchini kwa kipindi cha miaka minne amesema anajisikia fahari na bahati kupata fursa ya kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania na kwamba katika kipindi chake chote amepata ushirikiano mkubwa.
“Kwa kweli wakati wote wa uwakilishi wangu, nimekuwa nikipata ushirikiano wa kutosha wakati wa kutekeleza majukumu yangu jambo hili limenifurahisha sana na nitakuwa Balozi mwema kwa Tanzania,” amesema Balozi Al Maliki.
Balozi Al Maliki amewasihi watanzania kuendelea na utamaduni wao unaowafanya kuheshimika duniani kote hususani katika suala la umoja, amani na mshikamano bila ya kujali itikadi za kisiasa na dini.