Hakika maisha hayana mshindi, kwasababu binadamu tunazidiana kwa baadhi ya mambo na vitu tofauti na jambo zuri linalotia moyo ni kwamba, kila mtu anaweza kuamua kushindwa au kuwa mshindi wa maisha yake mwenyewe, kulingana na malengo na mipango mathubuti aliyojiwekea.
Ujasiri na kusimama badala ya wengine kwa manufaa ya jamii na Taifa pia ni jambo la kuigwa, na uhalisia ni kwamba, wakati wa kufanya maamuzi sahihi na kwa ushirikiano ni sasa na si kusubiri kesho kwani muda hauna urafiki na Wahenga walithibitisha hili kwa kusema “Wakati ni Ukuta”.
Haya ni baadhi ya maneno ya kishujaa ambayo yamesemwa na Mtandao wa Fahari ya Vijana, wakati wakizungumza na Dar24 Mbezi jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa katika maisha hauwezi kufanikiwa kwa kuwaumiza au kuwatendea wengine yale ambayo wewe haupendi kutendewa hivyo kuhimiza jamii na hasa Vijana kuangalia njia wanazopita, ili waweze kujipatia mafanikio bila kutoa maumivu kwa wengine.
“Jambo zuri na linalotia moyo ni kwamba, kila mtu anaweza kuamua kushindwa au kuwa mshindi wa maisha yake mwenyewe kulingana na malengo na mipango mathubuti aliyojiwekea katika kuyafikia malengo yake. Ujasiri na kusimama badala yaw engine kwa manufaa ya jamii na Taifa ni jambo la kuigwa, ni wakati wa kufanya maamuzi sahihi na kwa ushirikiano,” wamebainisha.
Mjadala huo, ulifanywa kwa pamoja kati ya Dar24 na Vijana hao wanaojishughulisha na masuala ya uelimishaji rika ambao baadhi yao ni Andew Chilongani, Omary Msata, Subira Ally, Shida Abdallah, Melea Daniel na Bahati Bega, ambao kwa umuhimu walisisitiza maadili mema ambayo yatasaidia ujenzi wa Taifa la kesho lililo bora, jema na imara.