Majaji wa Tunisia, wamegoma kwa muda wa wiki tatu huku wakifanya maandamano kupinga uamuzi wa Rais wa Tunisia, Kaiss Saied kuwatimua majaji 57 kwa madai ya ufisadi na kusema hatua ya kiongozi huyo ni mfano wa ziada wa unyakuzi wake wa madaraka.
Makamu wa Rais wa Chama cha Mahakimu wa Tunisia ( AMT), Aïcha Belhassan amesema Majaji wa Tunisia wanakusanyika katika mahakama zote za Jamhuri, ikiwa ni pamoja na Mahakama za utawala na fedha.
“Hatua hii inaendana na mgomo wa wazi unaofanyika katika vituo vyote vya Mahakama na itambulike kuwa baadhi ya Majaji waliofukuzwa kazi tayari wameanza mgomo wa kula kupinga hatua ya Rais,” amesema Belhassan.
Mahakimu hao, wanadai kuondolewa kwao kwa amri hiyo ya 35 ni kinyume na Katiba, kwani inashindwa kutoa haki ya msingi ya kujitetea na kuhatarisha uhuru wa mahakama.
Hata hivyo waandamanaji hao wamewasilisha ombi la kukutana na Mkuu huyo wa Nchi, lakini wanasema bado hawajapewa jibu na haijulikani kama ombi lao litaweza kufanyiwa kazi.
Rais Kais Saied, mwanzoni mwa mwezi huu wa Juni 2022, alimuita Waziri wa Sheria ili kuomba kusimamishwa kwa mishahara ya majaji hao wanaogoma.