Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafufua madarasa kwa ajili ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA) ili kusaidia kupunguza ongezeko la watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.


Ametoa agizo hilo leo Juni 9, 2021 wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania.


“Naagiza madarasa ya MEMKWA yahuishwe. Wakuu wa Mikoa na Wilaya suala la elimu ya watu wazima liwe sehemu ya ajenda zenu mnapofanya ziara. Fuatilieni kuiona elimu ya watu wazima inahuishwa ili kupunguza na ikiwezekana kuondoa kabisa tatizo la kutokujua kusoma na kuandika,” amesema Majaliwa.

Aidha, amewataka watumie madarasa hayo kuwezesha watu wazima wapate stadi mbalimbali pamoja na stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).


Waziri Mkuu amesema kuwa pamoja na kutekeleza majukumu mengine, Taasisi ya Elimu ya watu wazima iendelee kutekeleza kikamilifu jukumu lake la msingi la utoaji wa elimu ya watu wazima hadi katika ngazi ya Wilaya.

Baadhi ya washiriki wa kongamano la miaka 50 ya elimu ya watu wazima wakimsikiliza waziri mkuu Kassim Majaliwa


“Andaeni mkakati wa kusimamia utoaji mafunzo ya stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watu wazima badala ya kutoa astashahada, shahada na stashada tu. Idadi wa Watu wazima wasiojua kusoma imeongezeka hamna jinsi ya kukwepa jukumu lenu hili. Jipangeni upya ninafahamu fika Elimu ya Watu Wazima ni zaidi ya KKK,” amesema Majaliwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wataalam na wanataaluma wa Elimu ya watu wazima kutoa ushauri kuhusu namna ya kuboresha Vyuo vya kati vinavyotoa mafunzo mbalimbali ili kuzalisha wahitimu mahiri wanaohitajika katika viwanda na taasisi nyingine.


Akizungumza wakati alipotembelea  mabanda katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu ameitaka Taasisi ya Elimu ya watu wazima kuwatumia maafisa elimu ya watu wazima waliopo kwenye Halmashauri kwa kuwapelekea programu za elimu ya watu wazima ili wazitekeleze bila kujali kama wako kwenye mamlaka gani.


Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kutoa mafunzo ya elimu kwa watu wazima wanaohitaji kujiendeleza kitaaluma na kitaalam.


Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha wanawasaidia kujishughulisha kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na hatimaye kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Juni 10, 2021
Jaffar Haniu ateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu