Eva Godwin – Dodoma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza Kampuni zote zilizopewa kazi za upimaji wa viwanja kwenye Jiji la Dodoma na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, zilizo na zisizo na mikataba zichukuliwe hatua kali za kisheria.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo na kutafuta suluhisho.

Amesema, “tunatambua makampuni mengi hapa Dodoma ni ya watumishi wenyewe kama ambavyo imeelezwa kwenye ripoti. Mkurugenzi alikuwa na kampuni mbili, Mhasibu wake ana kampuni yake na wanazitumia kupima maeneo, kwa hiyo ni miradi yao.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Aidha, amewaagiza Wakuu wa Mikoa wahakikishe kuwa Kamishna Msaidizi wa Mkoa, Maafisa Mipango Miji wa Majiji, Halmashauri na Manispaa hawana sababu ya kuchukua watumishi wa muda kufanya kazi ya upimaji bali wafanye wao ili kuepusha mianya ya rushwa.

“Bwana Justin Albert, Freddy Mathias, Elias na Magige watafutwe, wachunguzwe na vyombo vya dola kuhusu nyaraka za Serikali walizonazo, na wazirejeshe nyaraka za Serikali wanazozitumia vibaya kwa kuendelea kuuza viwanja maeneo ya Jiji ya Ukanda wa Kijani, Mkonze, Ndachi, Chinyika, Ng’ong’ona na Mkalama,” amsema Majaliwa.

“Hawa ni vibarua, lakini wana ramani na wanavijua viwanja vyote. Wao wanachofanya ni kufanya mauzo halafu wanapeleka kwa watu wao pale Jiji na hati zinatoka. Kwa hiyo, watafutwe na wanyang’anywe zile nyaraka ili wasiendelee kuuza viwanja,” aliagiza.

Kocha wa Mwakinyo amjibu Promota Karigo
Mwamuzi apigwa marufuku kuchezesha England