Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi zote za Umma ambazo zinadaiwa na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kuhakikisha zinalipa madeni yao kabla ya Juni 30, 2017.
Ameyasema mapema hii leo Mjini Dodoma katika viwanja vya Bunge wakati wa uzinduzi wa huduma ya 4G LTE za kampuni hiyo ya simu kwa Mkoa wa Dodoma.
“Kuhusu shilingi Bil. 11.5 ambazo TTCL inazidai Taasisi mbalimbali za Umma, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, kaa na wadaiwa sugu wote, thibitisheni madeni husika kisha mkubaliane namna ya kulipa madeni hayo. Nijuavyo kila Wizara inatenga bajeti kwa ajili ya ankara za simu, sasa hayo malimbikizo yanatoka wapi?” amesema Kassim Majaliwa.
Aidha amezitaka Taasisi zinazodaiwa na TTCL kuhakikisha zinakamilisha madeni yao kabla ya kufikia Juni 30, 2017 ili kampuni hiyo iweze kufanya kazi ipasavyo na kuendana na ushindani wa kibiashara uliopo.
Vile vile ameitaka kampuni hiyo kujifunza kutoka katika mashirika ya Umma ya Simu kwenye nchi nyingine ambayo yanajiendesha kwa faida, kwa kuiga mbinu ambazo wanazitumia na kuziweka katika muktadha wa nchi ya Tanzania.
Hata hivyo, Majaliwa amempongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa pamoja na timu yake kwa hatua ambayo kampuni hiyo imefikia.