Serikali imewaagiza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Mlele kuhamia mara moja kwenye nyumba 11 zilizokuwa za wajenzi wa Barabara ya Inyonga-Mlele na kukabidhiwa kwa Halmashauri hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mlele mkoani Katavi baada ya kujionea mwenyewe kuwa zimetelekezwa na zinaharibika kwa kukosa uangalizi.
Amesema, “Watumishi wanahangaika hawana makazi, nyumba zimeachwa nyasi zimeota hadi kwenye korido. Watumishi wote wanaopaswa kuhamia katika nyumba hizi baada ya kumaliza mkutano huu kila mmoja aende kwenye yake na ahamie. Mkurugenzi naomba orodha ya majina ya watakaohamia.”
Watumishi ambao ameagiza wahamie kwenye nyumba hizo ni Afisa Usalama wa Wilaya (DSO), Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mlele (OCD), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mlele (DMO) na watumishi wengine wa Hospitali ya wilaya.
Nyumba hizo 11 zenye ukubwa tofauti kati yake mbili zinauwezo wa kuchukua familia nne kila moja na zimejengwa kisasa na zilikabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlele Novemba, 2022 na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), baada ya kukamilika kwa mradi wa Barabara.