Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa timu aliyoiunda kuchunguza tuhuma za ubadhirifu kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) imekamilisha kazi yake na imebaini madudu mengi zaidi.
Aidha, Waziri Mkuu aliivunja Bodi ya WETCU pamoja na Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Ameyasema hayo wakati wa ziara ya siku moja Mkoani Tabora alipokuwa akizungumza na wajumbe na wadau mbalimbali wa zao la Tumbaku.
“Nilikuja Tabora mara ya kwanza ili kuchukua hatua za dharura na leo nimekuja kuendelea na mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuwezesha kilimo cha tumbaku kiwe na tija kwa wakulima na ndiyo maana niliomba wakulima, wanunuzi wa tumbaku, vyama vya msingi vijitokeze ili viweze kutoa kero zinazowakabili,”amesema Majaliwa.
Ameongeza kuwa Tume aliyoiunda imefanya ufuatiliaji katika ngazi za benki lakini hakuna pesa yeyote iliyohifadhiwa katika akaunti za benki.
Vilevile, ameagiza kukamatwa kwa Mkurugenzi wa kampuni ya 4×4 Tanzania Limited, Faraz Yaseen na kuhojiwa ni kwa nini alihusika katika kuuza gari la mwaka 2008 na kubadilisha nyaraka ili lionekane ni la mwaka 2015.
Hata hivyo, Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri za Mkoa huo.