Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Pamba (CDTF) na amegiza wahusika wote wachunguzwe ili kubaini fedha walizokusanya zimetumikaje.

 Ametoa agizo hilo Desemba 22, 2017 wakati akizungumza na wadau wa zao hilo kwenye kikao alichokiitisha mkoani Shinyanga kufanya ufuatiliaji wa maagizo ambayo alikwishakuyatoa. Waziri Mkuu alishafanya vikao vitatu na wadau mbalimbali wa zao hilo.

 Amechukua uamuzi huo baada ya kubaini kuwa watendaji wa mfuko huo hawajatekeleza majukumu ya kuundwa kwa mfuko huo lakini pia majukumu yao yanaingiliana na yale ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).

 “Kuna CDTF katika zao la pamba lakini hakuna inachofanya ambacho kinawalenga wakulima moja kwa moja. Tunaiondoa CDTF na kazi zake kuanzia sasa zifanywe na Bodi,” alisema.

“Waziri wa Kilimo peleka timu ya ukaguzi kuona wamefanya nini hadi sasa. Tunataka Bodi ifanye kazi na iulizwe maswali kuhusu zao hili. Endapo kuna jambo halijafanyika, Bodi iwe na uwezo wa kutoa majibu si kusubiri tena mtu wa chombo kingine aje kutoa majibu,” alisema Waziri Mkuu.

“Kwa muundo huu, Mkurugenzi wa Bodi anakaa tu, wakati akisubiri kazi yake ifanywe na CDTF,” aliongeza.

Mfuko wa CDTF unaundwa na wajumbe sita ambao ni wawakilishi wa wakulima wawili, wawakilishi wa wenye viwanda vya kuchambua pamba wawili, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba na Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya Kilimo. 

Mfuko huu uliundwa mwaka 1999 na Bodi ya Pamba (TCB) ili uwashirikishe wadau wa zao hilo kuondoa matatizo yaliyojitokeza kwenye sekta hiyo baada ya Serikali kujitoa kwenye uendeshaji wa moja kwa moja wa mazao nchini ikiwemo uzalishaji na biashara kutokana na mfumo wa soko huria. 

Desemba mwaka jana, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alifikia uamuzi kama huo na kuamua kusimamisha shughuli zilizokuwa zinafanywa na Mfuko wa Kuendesha Zao la Korosho Nchini (CIDTF)ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za mfuko huo.

Akitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam, Waziri Tizeba alisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mfuko huo kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu pamoja na kuwapo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu utendaji wa mfuko huo.

 

Magazeti ya Tanzania leo Desemba 25, 2017
Dkt. Nchemba awakaanga wapinzani