Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza korosho zote zinazozalishwa katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi zisafirishwe kupitia badari ya Mtwara kwani serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika bandari hiyo kwa kuikarabati na kuipanua.

Hayo yamesemwa na Waziri mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kikao na wadau wa zao la korosho kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Sea View, iliyopo mjini Lindi.

Amesema kuwa Rais Samia amewaagiza viongozi wa bandari wapitie tozo zote zinazowakwaza wasafirishaji ili kuwavutia kuitumia bandari hiyo “tunataka wasafirishaji watumie bandari hii kusafirisha korosho kuanzia na msimu huu”.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa wakulima wakubali kupokea pembejeo kulingana na mahitaji yao na watalipia kulingana na idadi ya mifuko waliyochukua na sio shilingi 110 kwa kila kilo kama inavyelezwa .

“kila kilo ni gharama mno, lengo letu ni kuendelea kumpungumzia mzigo mkulima, msiogope kuchukua pembejeo” amesema Majaliwa

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wadau wote wa korosho nchini katika kufanikisha mkakati huo ikiwemo kutengeneza mashine za ubanguaji kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO).

“Tusisikie makato ya unyaufu kwasababu yanawafanya wanunuzi wahisikuwa wanaonewa, viongozi wa Serikali tusimamie hilo, hatutaki kusikia kuhusu tozo ya unyaufu” amesema Majaliwa

“wakulima wanakosa elimu ya namna ya kuliendesha zao hili, maafisa kilimo mlioko maofisini tokeni muende vijijini kuwaelimisha wakulima namna bora ya kulima mazao, wakati wote mnatakiwa kuwa shambani kuhakikisha wakulima wanalima kwa kuzingatia miongozo ya kilimo bora”.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima wa zao la Korosho kuwa na utaratibu wa kubangua korosho ili kupata faida zaidi badala kuziuza bila kuzibangua

Naye Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Wizara hiyo itaendelea kubuni na kusimamia mikakati itakayoongeza tija katika zao la korosho kwa kutoa pembejeo sahihi na kwa wakati  lengo likiwa ni kukidhi mahitaji ya masoko duniani .


Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Taleck amesema kuwa atashirikiana na viongozi wa mikoa ya Ruvuma na Mtwarakuhakikisha kwamba minada yote ya korosho inafanyika kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili kuwawezesha wananchi kiuchumi.


Mbunge wa Jimbo la Tandahimba Katani Ahmad Katani amesema kuwa amefarijika na kauli ya Serikali kuhusu korosho zote kusafirishwa kupitia bandari ya Mtwara kwani itasaidia kuongeza fursa za maendeleo katika mikoa ya kusini.

Mashindano ya kitaaluma yatawainua - Majaliwa
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Juni 7, 2021