Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa amegoma kufungua barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.2 iliyoko katika halmashauri ya wilaya ya Liwale mkoani Lindi kutokana na barabara kutokukamilika ikiwemo kuwekwa taa za barabarani kama mkataba wa ujenzi wake unavyoelekeza.
Ameyasema hayo leo, Oktoba 7, 2021 wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Idara ya Maji Kata ya Liwale Mjini ambapo palitengwa kwa ajili ya ufunguzi wa barabara hiyo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Lindi.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kila panapojengwa barabara na ikiwa inapita kwenye eneo la mji basi pawekwe na taa sasa hapa taa hakuna, hivyo barabara hii haijakamilika kwa hiyo siifungui naomba nikazungumze mengine pale na wananchi.” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara ya kutoka Nangurukuru hadi Liwale yenye urefu wa kilomita 231 ikiwa ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
Sambamba na hayo Waziri Mkuu Majaliwa akizungumzia suala la Elimu, ameuagiza uongozi wa wilaya ya Kilwa uhakikishe kuwa kati ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu katika halmashauri hiyo uhakikishe kijiji cha Kipindimbi kinapewa kipaumbele kwa kuboreshewa miundombinu na kuongezewa vyumba vya madarasa katika shule yao ya msingi.
Pia, Waziri Mkuu amewataka wazazi wahakikishe watoto wote wenye umri wa kwenda shule wakiwemo watoto wa kike wanapelekwa kwani Serikali imeondoa michango iliyokuwa inakwaza wananchi.