Maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu nchi kujitosheleza kwa uzalishaji wa sukari yameonesha dalili njema baada ya uongozi wa kiwanda cha sukari cha Kagera, kuongeza uzalishaji na kufikia tani 110,000 kutoka tani 60,000.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hii leo Oktoba 15, 2022 katika ziara yake ya kukagua upanuzi wa mashamba ya miwa na mitambo na iliyoongezwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Sukari Kagera, kilichopo Misenyi Mkoani Kagera.
Amesema, kitendo cha kampuni hiyo kuendelea kuweka mikakati ya kuboresha na kukuza uwekezaji ni kizuri, kwani kitaongeza kiwango cha uzalishaji wa sukari nchini, na kuipunguzia Serikali gharama ya kuagiza Sukari kutoka nje.
“Uwepo wa kiwanda hiki ni fursa ya kiuchumi kwa wakazi waishio katika vijiji jirani na kiwanda hicho ambao wanajiajiri kupitia kilimo cha miwa kwa kuwa wana uhakika wa soko kiwandani hapa, endeleeni kuiunga mkono Serikali kwa kuongeza fursa za ajira kupitia kiwanda chenu.” amesema Majaliwa.
Aidha, Majaliwa pia amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Kanali Wilson Sakulo kuwahamasisha wananchi wa vijiji 13 vinavyozunguka kiwanda hicho, kulima zao la miwa kwa wingi ili kuweza kujiongezea kipato na kuongeza idadi ya malighafi inayohitajika kiwandani hapo.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Sukari Kagera, Seif Ali Seif alisema kiwanda kimefanikiwa kuongeza uzalishaji na wanatarajia kuzalisha tani 110,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu tofauti na miaka mitano iliyopita ambapo walikuwa wanazalisha tani 60,000 kwa mwaka na wana lengo la kuzalisha tani 300,000 na kwamba Kiwanda kimeajiri watumishi 10,000.