Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mkoa wa Lindi mwaka huu.
Amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imefanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na kufuta michango yote ya hovyo iliyokuwa ikiwakera wazazi na walezi.
Ametoa pongezi hizo katika mkutano wa kuwapongeza walimu wa wilaya ya Ruangwa na baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu.
Aidha, kufuatia matokeo hayo mazuri Waziri Mkuu kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa imetoa zawadi mbalimbali kwa Kata tatu bora zilizofanya vizuri, shule 10 bora, walimu ambao wanafunzi wao wamepata daraja A katika masomo mbalimbali wanayofundisha pamoja na wanafunzi 10 bora.
“Nawapongeza kwa sasa mimi kitaaluma ni mwalimu hivyo nafahamu ili mwanafunzi apate matokeo mazuri ni lazima mwalimu afanye juhudi kubwa zitakazomuwezesha mwanafunzi kufaulu masomo yake.”amesema Majaliwa.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi wa wilaya ya Ruangwa, Mwalimu Selemani Mrope amesema kuwa kuanzia mwaka 2015 hadi 2017 hali ya ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba haikuwa nzuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya utoro.