Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wana Lindi na wana Ruangwa watumie fursa zilizopo ili kufanikisha maandalizi ya sherehe za Maulid na Baraza la Maulid Kitaifa mwaka huu.

Majaliwa ametoa wito huo leo Novemba 5, 2017 wakati akizungumza na viongozi wa dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Lindi na wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.

Amesema sherehe hizo zitafanyika Desemba mosi kwa mkesha wa Maulid na kufuatiwa na Baraza la Maulid litakalofanyika Desemba 2, saa 3 asubuhi kwenye viwanja vya shule ya msingi Likangale.

Amewataka wana-Ruangwa waharakishe kujenga nyumba za kulala wageni na sehemu za kula ili waweze kupokea ugeni huo mkubwa wa kitaifa. “Kila mmoja anayeona hapo kuna fursa, ni lazima aitumie vizuri,” alisisitiza.

“Kwa niaba ya wana-Ruangwa, tunamshukuru Mheshimiwa Mufti na Baraza la Maulamaa kwa kuridhia sherehe hizi zifanyike kitaifa hapa wilayani kwetu. Nitumie fursa hii kuwaomba Waislamu wote tuungane katika sherehe hizi licha ya tofauti za madhehebu yetu tuliyonayo,” amesema.

Majaliwa amesema kuwa uamuzi huo wa BAKWATA ulitangazwa kwenye Baraza la Maulid lililofanyika Singida, mwaka jana ya kwamba wameamua kuadhimisha sherehe hizo kwenye ngazi ya wilaya badala ya kuwa inafanyika makao makuu kila mwaka.

Pia ametumia fursa hiyo kuwaarifu viongozi hao kwamba maandalizi yanaendelea na kwamba vifaa mbalimbali kama mchele, vitoweo, unga wa ngano, sukari, maji, juisi, mahema, mikeka na mazulia vimekwishapatikana.

“Ninaomba Kamati ya Uhamasishaji iifanye kazi hii kwa kutambua kuwa jambo hili si la kwenu peke yenu, bali linaungwa mkono na Serikali, na hii ni kwa sababu Serikali yenu inafanya kazi kwa karibu sana na viongozi wa dini,” alisema.

Amesema misingi ya amani katika nchi hii imejengwa na mahubiri ya viongozi wa dini.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji, Sheikh Ali Mohammed Mtopa aamesema Ruagwa iko tayari na imepokea wito huo wa kitaifa. “Tunakuhakikishia wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wawakilishi wa Mufti waliopo hapa kwamba tumepokea hiyo heshima,” amesema.

Na kwa upande wake Mkurugenzi wa Itifaki kutoka BAKWATA Makao Makuu na Msimamizi wa Malidi za Kitaifa, Sheikh Mohammad Nassir ambaye alisema wana Ruangwa an wana Lindi wanalo jukumu la kuhamasisha watu washiriki sherehe hizo.

“Hamasa haitatoka Morogoro au Dar es Salaam bali hapahapa Lindi. Tunataraji watu wasiopungua 10,000 watahudhuria sherehe hizi za Maulid kutoka wilaya zote za mkoa wa Lindi na hii ni mbali wawakilishi kutoka kila mkoa wapatao 100 -150,” amesema.

 

RC Wangabo “Hakuna Mwandishi wa habari atakayefungwa wala kuzuiwa kufanya kazi yake,”
Magazeti ya Tanzania leo Novemba 6, 2017