Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Taasisi ya kilimo cha bustani nchini (TAHA), kuongeza uzalishaji wa mazao ya bustani ili kupunguza uagizaji wa bidhaa ziazotokana na mazao ya bustani kutoka nje ya nchi.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Desemba 5, wakati akitoa hotuba katika kongamano la uwekezaji na biashara ya mazao ya bustani ambapo amesema ongezeko la uzalishaji wa mbogamboga na matunda ambayo hutoa juisi au majimaji litafungua milango ya sekta nyingine nchini.
Majaliwa ametoa wito kwa wadau kutoka nje ya nchi waliohudhuria kongamano hilo kutumia fursa zilizopo katika kilimo cha bustani nchini kwa kushiriki kilimo, kuanzisha viwanda vya uchakataji mazao ya bustani na kutafutia masoko bidhaa za mazao ya bustani zinazozalishwa nchini.
Aidha, Waziri Mkuu ameeleza kuwa serikali katika kuunga mkono juhudi za wakulima imepunguza kodi na kufuta tozo 168 zilizokuwa zikitozwa awali katika sekta ya kilimo.
Majaliwa pia, ametoa wito kwa Wizara ya kilimo, TAHA na wadau mbalimbali wa kilimo kutoa elimu kwa wakulima wa mazao ya mbogamboga, viungo, maua na matunda ili kuongeza uwezo wa watanzania kuleta ushindani katika soko la kimataifa.