Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa amekabidhi Jenereta katika kituo cha afya cha Mkowe halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi, ambalo litasaidia kufua Umeme Wa dharura kituoni hapo.
 
Akizungumza na Wananchi pamoja na wauguzi kituoni hapo kwa niaba ya Waziri mkuu wakati Wa hafla hiyo Naibu waziri Wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa amefurahishwa na maboresho yaliyofanyika katika kituo hicho kwa kuweza kufanya upasuaji kwa akina mama wajawazito.
 
Aidha, Mgalu amelitaka shirika la umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Lindi kuendelea na uboreshaji wa upatikanaji wa umeme katika mkoa huo.
 
Awali akitoa taarifa ya kituo hicho Mganga mfawidhi wa kituo hicho, Paulo Mbinga amesema kuwa kituo cha afya Mkowe ni miongoni mwa vituo vya afya vinavyonufaika na mpango wa serikali wa kuimarisha miundombinu ya vituo vya afya nchini unaolenga kuviwezesha vituo vya kutoa huduma za dharura kwa kina mama wajawazito.
 
Amesema kuwa kituo hicho kwa sasa kinahudumia jumla ya wananchi 5,224 kwa kata ya Mkowe pamoja na zile za jirani kama chienjele, Nandagala, Likunja, Namalolo na Mnacho ambapo jumla ya wagonjwa 74 hufika kituoni hapo kwa Siku kwa ajili ya matibabu .
 
Hata hivyo, Dkt. Mbinga amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo la Ruangwa kwa kuwasaidia Jenereta katika kituo hicho ambacho kwa kiasi kikubwa litasaidia utoaji wa huduma kwa wagonjwa pindi umeme utakapokatika.

Video: Mfumo wa Ada Lipa wazidi kuwarahisishia watanzania ulipaji ada mashuleni
Nditiye akabidhi Kompyuta 25 Ludewa