Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi wa Makumbusho ya Taifa kwa kuchora ramani ya Tanzania katika Kijiji cha Makumbusho ambayo itatumika kwenye ujenzi wa nyumba za utamaduni wa makabila mbalimbali nchini.

Amesema uamuzi huo utarahisisha watu kufika kwa urahisi katika nyumba za tamaduni za mikoa yao kwa kuwa watakuwa wanatumia ramani Tanzania.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa mkoa wa Lindi kwenye kikao cha kujadili maandalizi ya Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania katika Kijiji cha Makumbusho, jijini Dar es Salaam.

“Kwa kutumia ramani hii kila mkoa utaweza kufika kwenye eneo lake kwa kutumia ramani ya Tanzania na mkoa wa Lindi tayari umeshaonyeshwa eneo lake kwa ajili ya ujenzi wa nyumba inayozingatia utamaduni wetu,” amesema Majaliwa

Aidha, amesema kwa tamaduni za makabila ya mkoa wa Lindi nyumba zote hujengwa kwa udongo na kuezekwa kwa makuti upande wa maeneo ya pwani ya upande mwingine huezeka kwa nyasi, ambapo aina zote zitajengwa ili kuwakilisha tamaduni za wakazi wa mkoa huo.

Hata hivyo, Majaliwa amewaasa wananchi wa mkoa wa Lindi ambao kwa mwaka huu ndio waandaaji wa tamasha hilo wadumishe mshikamano wao ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea katika kuboresha maendeleo.

 

Wapinzani wasijisumbue, ushindi uko palepale- Nape Nnauye
Kangi Lugola achukua maamuzi magumu baada ya ajali ya Kigwangallah