Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini katika nyanja mbalimbali ili kukuza na kuimarisha ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Agosti 12, 2022 alipomuwakilisha Rais Samia katika ufunguzi wa Jengo la Makao Makuu ya Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) katika Chuo cha Biblia Miyuji, Dodoma.
Jengo hilo litakuwa na ofisi mbalimbali za kiutendaji za TAG pamoja na kutoa mafunzo ya uzamili na uzamivu kwa viongozi na wachungaji mbalimbali kutoka Bara la Afrika na maeneo mengine duniani.
“Sote tumeshuhudia jinsi Serikali inavyoweka mazingira mazuri ya kuwekeza kwa ujenzi wa miundombinu muhimu ya barabara na madaraja, reli ya kisasa, vivuko, meli na usafiri wa anga. Jitihada hizi zote pamoja na kuimarisha uzalishaji wa umeme, gesi na maji hapa nchini zinafanyika kwa lengo la kuboresha ustawi wa maisha ya Tanzania.” amesema Waziri Mkuu.
“Serikali inaelewa kwamba Maendeleo ya nchi yanahitaji ushiriki wetu sote. Tukiimarisha ushirikiano na kila mtu, tutaleta maendeleo ya Taifa. Kwa kuzingatia hayo, Serikali imekuwa ikishirikiana na Sekta binafsi zikiwemo Taasisi za dini katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa.”
Amesema kanisa la TAG, pamoja na taasisi nyingine za kidini zimekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma mbalimbali zinazogusa jamii kama elimu, afya na huduma nyingine muhimu kwa jamii ambazo Serikali pekee isingeweza kuzifikisha kwa wananchi mara moja.
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya TAG ya kucheleweshwa kumilikishwa ardhi katika eneo la Chigongwe, amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru ahakikishe suala hilo linashughulikiwa haraka na ndani ya siku saba awasilishe taarifa kwake. TAG linataka kujenga chuo kikuu katika eneo hilo.