Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kukamilisha zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika maeneo yote ya hifadhi ifikapo Desemba 30, 2017.

Ametoa agizo hilo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Ulyankulu, John Kadutu, alilouliza kuhusu kuwepo kwa migogoro ya mipaka kati ya wananchi na hifadhi ambapo baadhi ya wananchi wanaendesha shughuli za kijamii ndani ya hifadhi.

Kadutu alitaka kujua hatua zilizofikiwa na Serikali katika uwekaji wa alama za mipaka katika maeneo mbalimbali ya hifadhi ili kuwaondolea wananchi usumbufu.

“Wizara ifanye mapitio ya maeneo yote ya hifadhi ambayo bado hayajawekewa alama za mipaka na kukamilisha zoezi hilo ifikapo tarehe 30, Desemba, 2017.”

Aidha, Waziri Mkuu amesema wananchi wanaoshi katika maeneo yaliyoko ndani ya hifhadhi wawaache wataalamu wakamilishe zoezi hilo na baada ya kukamisha Serikali itafanya mapitio na kisha kutoa maamuzi kwa manufaa ya Taifa.

Waziri Mkuu amesema sheria namba moja ya Ajira za Wageni ya mwaka 2015 inaruhusu utoaji wa vibali vya ajira kwa wageni kwa muda wa miaka miwili.  “Hata hivyo vinaweza kuongezwa kulingana na mahitaji hadi kufikia vipindi viwili.”

Hata hivyo, Serikali imewapa masharti wageni wanaoomba vibali vya kufanya kazi nchini kuandaa mpango wa kuwarithisha ujuzi Watanzania ili kuchukua nafasi za wageni hao mara baada ya muda wa vibali vyao kumalizika.

 

 

RC Rukwa azitaka halmashauri kushirikiana na SIDO
Kigogo wa Takukuru apandishwa kizimbani