Balozi wa Tanzania Nchini Malawi, Benedict Mashiba ametakiwa kuhakikisha anadumisha na kuimarisha uhusiano wa Kidplomasia uliopo baina Malawi na Tanzania ili inchi hizo ziendelee na ushirikiano uliopo.
Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dar es slaam na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuta na balozi huyo, ambapo amemtaka ahakikisha anaboresha shughuli zote za Kidiplomasia baina ya nchi hizo.
Amesema kuwa Balozi anatakiwa kuhakikisha anatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, ukiwemo Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo nchini hususani katika sekta ya viwanda.
Aidha, Majaliwa ameongeza kuwa licha ya kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii pia amemtaka kuboresha biashara baina ya Tanzania na Malawi kwa kutumia meli mbili za mizigo za Mv. Ruvuma na Mv. Njombe alizozizindua hivi karibuni wakati wa ziara yake.
Hata hivyo, amesema kuwa ni vyema Balozi huyo kutenga muda wa kukutana na kufanya mazungumzo na Watanzania waishio nchini Malawi na kuwasisitiza kuishi kwa kuzingatia sheria za nchi husika. Pia kuwaunganisha pamoja na kuwashauri kuja kuwekeza nchini.
Kwa upande wake Balozi Mashiba amesema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuboresha ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi.