Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa tayari amewasili Nairobi, Kenya kuhudhuria Mkutano wa Mkuu wa Sita wa Wakuu wa Nchi wa TICAD (TICAD VI) kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli utakaofanyika Agosti 27 – 28, mwaka huu.

Waziri Mkuu mapema leo (Ijumaa, Agosti 26, 2016) amekutana na viongozi wakuu mbalimbali wa makampuni ya kibiashara kutoka Japan ambao wamekuja kuhudhuria mkutano huo.

Majaliwa amekutana na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Chiyoda Corporation, Bw. Tadashi Izawa ambapo katika mazungumzo yao,pamoja na kuangalia fursa nyingine katika sekta ya gesi Tanzania, kampuni hiyo imekubali kutoa mafunzo ya kujenga uwezo wa wataalamu kwa sekta ya gesi hususan usindikaji wa gesi kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi (Liquefied Natural Gas).

Tadashi Izawa amemweleza Waziri Mkuu kwamba wamefurahiswa na taarifa za ugunduzi wa gesi ya Helium hapa nchini Tanzania na kwamba kampuni yake ina teknolojia na uzoefu wa muda mrefu katika kutekeleza miradi ya gesi (Gas value Chain Planning and Execution).

“Tunao uzoefu wa muda mrefu, pia tunazo teknolojia za kuendeleza sekta ya gesi ikiwemo Helium kwa mfano ujuzi wa kutenganisha gesi asilia na helium (Separation of Natural Gas and Helium). Tumetekeleza miradi ya namna hii nchini Qatar ambayo kwa sasa ni ya pili kwa uzalishaji wa gesi hiyo duniani ikitanguliwa na Marekani,” amesema.

Pia, amesema mafunzo hayo yatafanyika kuanzia mwakani na yatalenga vijana wasiopungua 10 kutoka Tanzania ambao wamehitimu shahada za uhandisi kwani wameshafanya hivyo kwa vijana wanane kutoka Msumbiji.

Majaliwa alimshukuru Tadashi Izawa kwa mpango wao wa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania lakini akamtaka pia waangalie uwezekano wa kuwasaidia vijana wanaotoka maeneo husika yenye gesi ili wapatiwe mafunzo ambayo yatawawezesha kumudu baadhi ya kazi kwenye viwanda vya kusindika gesi.

pia, Waziri Mkuu amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Hiroshi Kato na kujadiliana mambo kadhaa yakiwemo ya nishati na miundombinu.

Katika mazungumzo hayo, Bw. Kato alimweleza Waziri Mkuu nia ya shirika hilo kuendelea kusaidia miradi mbalimbali ya kilimo hapa nchini na hasa katika sekta za afya, maji, kilimo na miundombinu ambazo imekuwa ikijihusisha nazo kwa muda mrefu sasa.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mathias Chikawe alimwoba makamu wa Rais huyo waangalie uwezekano wa kuwekeza kwenye sekta za nishati na miundombinu ya mkoa Dodoma hasa katika kipindi ambacho Serkali imeamua kuhamia huko.

“Tunaomba muangalie sana suala la kuendeleza nishati ya umeme kwani nchi yetu imeamua kuwa nchi ya viwanda. Tutahitaji kuwa na umeme wa kutosha kuendesha viwanda vya usindikaji bidhaa zetu, lakini pia si mbaya mkiangalia suala la kuboresha miundombinu ya barabara na usafirishaji katika mji wa Dodoma,” – Mathias Chikawe

Video: JICA kusaidia ujenzi wa miundombinu Dodoma
Video: Msanii mkali wa Nigeria ‘YCEE’ kuizulu Dar