Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amenunua hisa za kampuni ya Vodacom Tanzania zenye thamani ya shilingi milioni 10 pamoja na nyingine za shilingi milioni 10 kwa ajili ya mke wake, Mary Majaliwa.
“Hii ni fursa kwa kila Mtanzania, kwa viongozi kwa taasisi na mashirika ya umma, taasisi binafsi, wajasiriamali wadogo kama akinamama lishe au madereva wa bodaboda. Watanzania walioko nje ya nchi (Diaspora) nao pia wanunue hisa kwani watakuwa wanachangia uchumi wa nchi na wakati huo wanaweka akiba nyumbani,” ameongeza.
Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mbele ya wakuu wa Masoko ya Hisa na Dhamana, Soko la Hisa la Dar es Salaam, viongozi wa Baraza la Uwezeshaji na kampuni ya Vodacom katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam, ambapo amewasihi Watanzania walioko ndani na nje ya nchi wachangamkie fursa ya kununua hisa hizo ili waweze kuwa wamiliki wa kampuni kupitia hisa zao.
Amesema watumishi wa umma wamepewa ya kununua hisa hizo kupitia mipango iliyowekwa na Makatibu Wakuu wao lakini pia amewasihi viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi wachangamkie fursa hiyo ili nchi iweze kupata kodi kupitia makampuni hayo.
Awali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango uwekezaji kwenye hisa ni njia mojawapo ya kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa nchi.
“Huko mtaani ukisema uchumi wa nchi unakua, watu wanabisha wakidai kuwa hawaoni unakua kwa sababu hawana fedha mifukoni. Hii ni fursa nyingine ya kuwawezesha kukua kiuchumi, ninaomba waichangamkie,” amesema.
Mpango amesema anatoa ombi maalum kwa wafugaji kukubali kuuza mifugo yao na kununua hisa ili kupunguza idadi ya mifugo yao, jambo ambalo alisema litapunguza migogoro baina yao na wakulima.
“Wakulima wa vitunguu, alizeti, maua au wafugaji wa samaki nao pia wanaweza kununua hisa na kuwa na mitaji kwa ajili ya shughuli zao. Ninawasihi wote watumie fursa hii ili kumiliki kampuni,” amesema.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana, Nassama Masinda alisema amefurahishwa kuona Waziri Mkuu akinunua hisa za kampuni ya Vodacom katika soko la awali.
Amesema uuzwaji wa hisa hizo ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kuwa wamiliki wa makampuni ya simu za mikononi hapa nchini. “Marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta sura ya 306 yanazitaka kampuni za simu na mawasiliano ya kielektroniki kuuza si chini ya asilimia 25 ya hisa zao kwa umma wa Tanzania kupitia masoko ya mitaji (IPO).”
Baada ya hapo hisa hizo zinapaswa kuorodheshwa kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, sura ya 79. Kampuni ya Vodacom ilitoa hisa milioni 560 kwa umma kwa bei ya sh. 850 kila moja na hivyo kutarajia kukusanya sh. bilioni 476.
Amesema hivi sasa, wawekezaji kwenye masoko ya mitaji ni watu 500,000 tu ikilinganishwa na Kenya ambayo ina wawekezaji milioni 1.7; Uganda (40,000) na Rwanda (14,000). “Vodacom ina wateja milioni 6.2, iwapo nusu ya wateja wake wote watashiriki ununuzi wa hisa, idadi ya wawekezaji kupitia masoko ya mitaji na dhamana itaongezeka kwa asilimia 1,140. Na haya yatakuwa ni mageuzi makubwa katika sekta ya masoko ya mitaji si hapa nchini tu bali katika Afrika Mashariki,” amesema.