Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa ya Singida, Mbeya, Iringa na Dodoma wawasimamie wananchi wao na kuhakikisha hakuna shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya vyanzo vya maji.
Ameagiza vifanyike vikao vya ujirani mwema ili wananchi waelimishwe umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na ni marufuku kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo.
Majaliwa amesema hayo leo Januari 19, 2017 alipozungumza na watumishi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera alipotembelea bwawa la Mtera akiwa njiani kwenda mkoani Njombe kwa ziara yake ya kikazi, na ametoa agizo hilo baada ya Kaimu Meneja wa Kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera, Mhandisi Edmund Seif kutaja baadhi ya changamoto zinazokikabili kituo hicho kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji.
“Marufuku wafugaji kuingiza ng’ombe ndani ya vyanzo vya maji na badala yake utafutwe utaratibu wa kuwachimbia mabwawa pembeni. Pia wakulima nao wazuiwe kulima ndani ya vyanzo vya maji. Lazima tushirikiane kulinda vyanzo vyetu,” amesema.
Akitaja baadhi ya changamoto kwa Waziri Mkuu, Mhandisi Seif amesema kituo hicho cha Mtera kinazalisha megawati 80 kwa siku ambazo zinaingizwa kwenye gridi ya Taifa. Alisema bwawa hili kwa sasa lina maji ya kutosha kuzalisha umeme hadi msimu ujao wa mvua.
Mhandisi hiyo alisema bwawa hilo linategemea kupata maji kutoka mto Ruaha Mkuu, mto Ruaha Mdogo na Vyanzo vyote hivyo vinaathiriwa na shughuli za kibidamu ambapo watu wanalima na kuingiza mifugo.
Pia, Majaliwa ametembelea shamba la Igingilanyi ambalo ni moja kati ya mashamba matatu ya kufugia ng’ombe yanayomilikiwa na kiwanda cha kuzalisha bidhaa za maziwa ya Asas kilichoko mkoani Iringa.
Akiwa shambani hapo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia vizuri mgawanyo wa ardhi ndani ya halmashauri zao pamoja na kusimamia mipaka kati ya wilaya na wilaya.
“Wekeni mipango bora ya matumizi ya ardhi. Pimeni ardhi na mgawe hati ili kumaliza migogoro ya ardhi hata kwa waliopewa mashamba makubwa nao wapimiwe na ardhi yao na wapewe hati kwa mujibu wa muda uliowekwa kisheria,” amesema.