Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewapiga marufuku Mawaziri na Naibu Mawaziri kujiepushe na utoaji wa matamko yasiyotekelezeka ili kuepuka mikanganyiko Serikalini.

Ameyasema hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika mjini Dodoma, ambapo amesema kuwa ni vyema viongozi hao kabla ya kutoa matamko wakajiridhisha iwapo jambo hilo halitaleta athari za kibajeti na kisera na kama lipo katika bajeti za wizara zao.

Majaliwa amewataka viongozi hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi ili kuithibitishia jamii kuwa Rais Dkt. John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao kiutendaji.

“Tunao wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii ili kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli na wananchi wote kwa ujumla.”amesema Majaliwa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa kusikiliza hoja na shida za Wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni, huku akiwataka wafanye ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao kwa kuwa wao ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

 

Bomu laua wanafunzi sita Kagera
Video: Deontay Wilder atamba kumpiga Anthony Joshua