Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika utunzaji wa misitu kwa kutekeleza azma ya uhifadhi na uendelezaji misitu kwa vitendo.
Amesema hayo leo (Jumatano, Juni 01, 2022) wakati akizindua zoezi la upandaji miti katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma. “Watanzania tuendelee kupanda na kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa miti na misitu kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu.
Amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) imeendelea kuratibu utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji na utunzaji wa miti inayotekelezwa nchini kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.
“Katika kipindi cha mwaka 2020/21, Halmashauri 27 kati ya 184 zilivuka lengo la kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka ambapo idadi ya miti 202,923,907 ilipandwa na miti 165,501,119 ilistawi, ambayo ni sawa na asilimia 81.6,” amesema.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kushirikiana na timu inayosimamia na kuratibu ujenzi wa Mji wa Serikali zihakikishe miti ya aina mbalimbali inapandwa na kutunzwa katika maeneo yaliyoainishwa ikiwemo kuhakikisha mifumo ya umwagiliaji inafungwa mapema iwezekanavyo.
Pia, amewaagiza wataalamu wa mazingira waielimishe jamii juu ya upandaji bora wa miti kwa kuzingatia hali ya hewa ya eneo husika ili upandaji huo uwe na tija.
“Kumekuwa na jitihada nyingi sana za upandaji miti, nisisitize miti ipandwe kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wetu. Nitoe wito kwa wataalamu kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu bora ili upandaji miti uwe na tija zaidi,” amesema Majaliwa.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jaffo amesema kuwa wamejipanga kuendelea kuipa kipaumbele ajenda ya utunzaji wa mazingira “Hatuwezi kuupeleka uchumi wetu mbele kama tutadharau na kuacha kutunza mazingira yetu,”
Kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani itakayoadhimishwa Juni 05, 2022 ni ‘Tanzania ni Moja Tu; Tunza Mazingira’.