Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa amesema ili kuleta maendeleo endelevu ya viwanda, kuongeza biashara na kutengeneza ajira, nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zinapaswa kuwekeza katika uunganishaji na uwianishaji wa viwango mbalimbali vya TEHAMA.

Amesema hatua hiyo itasaidia kutatua changamoto za maendeleo ya miundombinu na muingiliano wa mawasiliano nje ya mipaka ya nchi na kikanda. “Changamoto hizo zinajumuisha maunganisho ya njia kuu za mawasiliano kati ya nchi jirani, kuyafanya mawasiliano ya kikanda yabaki ndani ya kanda, kuvuka mipaka ya nchi, upangaji wa bei pamoja na uwianishaji wa viwango.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa SADC wa sekta ya TEHAMA,  uchukuzi na hali ya hewa pamoja na kongamano maalumu la Mawaziri, unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Majaliwa amesema kwa kipindi hiki, nchi wanachama zinapaswa kuhakikisha kuwa utekelezaji unalenga katika teknolojia zinazochipukia kwenye utoaji wa huduma za posta sambamba na kuanzisha huduma na bidhaa mpya ambazo zitakidhi mahitaji ya sasa ya wateja na kuhamasisha biashara mtandao.

“Katika kufanikisha hili, ni muhimu kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mkakati wa Posta wa SADC wa mwaka 2017-2020 ambao uliridhiwa mwezi Septemba, 2017.” amesema Majaliwa

Aidha, Waziri Mkuu amesema ili kufikia mtangamano wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji, mkutano huo unapaswa kuzungumza namna gani nchi wanachama zinaweza kuwianisha sera, viwango, mifumo ya sheria katika maeneo ya barabara, reli, usafiri wa anga, usafiri wa majini, pamoja na hali ya hewa.

“Tanzania imeweza kuboresha miundombinu ya bandari pamoja na mifumo ya uendeshaji ili kusaidia nchi za SADC ambazo hazipakani na bahari nazo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Malawi pamoja na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za Jamhuri za Uganda, Rwanda na Burundi.” ameongeza Majaliwa

Mkutano huo unahudhuriwa na Mawaziri wa Sekta ya TEHAMA, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa kutoka nchi za Angola (4), Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (2), Msumbiji (1) Zambia (3), Afrika Kusini (2), Lethoto (1), Zimbabwe (2) na Tanzania inawakilishwa na Mawaziri watano na Naibu Waziri Mmoja, akiwemo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye ndiye Mwenyekiti wa Mkutano huo.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 20, 2019
Kaburu, Aveva wafutiwa shtaka la kutakatisha fedha