Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, amewataka watendaji wa Serikali  wahakikishe wanawasimamia vizuri wakandarasi wanaojenga miradi mbalimbali nchini zikiwemo barabara ili viwango vyake vilingane na thamani halisi ya fedha zinazotolewa.

Ameyasema hayo alipokuwa akizindua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kwerekwe/Fuoni yenye urefu wa kilomita 4.01 iliyogharimu sh. bilioni 10.07 zilizotolewa na Mfuko wa Barabara.

Majaliwa amezindua barabara hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli ikiwa ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

“Serikali imedhamiria kuboresha mawasiliano kwa kujenga barabara zetu kwa kiwango cha lami. Hatatutakubali kuona mtu anaharibu miundombinu hii tunayoijenga kwa gharama kubwa ikiharibiwa lazima tuilinde ili iweze kutunufaisha wote,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amewataka madereva wote kuhakikisha wanakuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani ikiwemo kusimama kwenye alama za kuvukia watembea kwa miguu na atakayekaidi achukuliwe hatua.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe amesema barabara hiyo ni sehemu ya awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Kwerekwe hadi Tunguu.

 

Mbunge wa Chadema atupwa jela
Video: Nape amkabidhi bendera ya Taifa Diamond kutumbuiza AFCON 2017, nchini Gabon