Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewapa maagizo viongozi wa Mkoa na Wilaya kuhakikisha pembejeo za kilimo zinazotolewa na Serikali kwa njia ya ruzuku zinawafikia walengwa na hakuna ubadhirifu unaofanywa, huku akisema Serikali haitawatupa wakulima wa zao la tumbaku na kuwataka waongeze uzalishaji kwani soko la uhakika lipo.
Kauli hiyo, imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Nasuli, Ruvuma ukiwajumuisha wakulima, wanunuzi, wenye viwanda, maafisa kilimo, wasambazaji mbolea na wenye mabenki.
Amesema, “Hakikisheni pembejeo za kilimo zinazotolewa na Serikali kwa njia ya ruzuku zinawafikia walengwa na hakuna ubadhirifu, Serikali yenu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitawatupa mkono, nami kwa maelezo yenu ya leo nitamfikishia salamu Mheshimiwa Rais kuwa mmeazimia mtalima zaidi tumbaku.”
Aidha, amewataka Viongozi hao wa mkoa wa Ruvuma, kushirikiana na Wizara ya Kilimo kusimamia upatikanaji wa huduma za ugani kwa wakati, ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na kuitaka Bodi ya Tumbaku kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili kufikia malengo yaliyowekwa na kusisitiza kuwa wakulima wa tumbaku waelimishwe kufuata mbinu bora za kilimo.