Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wathamini wote kuwa waadilifu, wenye weledi na wazingatie miiko ya taaluma katika kazi zao za kila siku, kwani wao ni watu muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya Taifa.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Mwaka wa Wathamini unaofanyika kwa siku mbili katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Amesema, “mnapaswa kuwa waadilifu na kuzingatia thamani halisi ya ardhi, jengo au chochote kinachofanyiwa uthamini, Kazi ya uthamini si ya wababaishaji au vishoka, hivyo basi kila mthamini hana budi kuthamini na kuheshimu taaluma yake.”
Majaliwa amesisitiza kuwa, “wapo baadhi ya wathamini ambao si waadilifu kwa kushirikiana na watendaji wengine hutoa makadirio ambayo hayawiani na thamani halisi. Vitendo hivyo husababisha kupoteza mapato ya Serikali lakini pia kuwanyima haki wale wanaostahili kupata haki.”
Aidha, amewataka watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hususani wathamini washirikiane na sekta binafsi kufanya kazi za uthamini.
“Tumieni fursa ya uwepo wa wathamini binafsi ili kutoa huduma bora na ya haraka hapa nchini, kufanya hivyo mtakuwa mnatekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ushirikishaji wa sekta binafsi kwa maendeleo ya Taifa,” amesema.