Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi waimarishe uhusiano na urafiki na watoto wao, ili waweze kupata taarifa za viashiria na uwepo wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto huku akiwaomba viongozi wa dini kuendelea kuwakumbusha waumini wao wazingatie maadili na kushiriki kikamilifu kuwalea watoto kiroho, kuhimiza uadilifu na kuepuka vitendo visivyokubalika katika jamii.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akihitimisha hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wakijadili Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.

Amesema, “Jengeni utamaduni wa kutenga muda wa kuwasikiliza watoto ili kujua kinachoendelea katika maisha yao ya nyumbani, mtaani na shuleni  na kuchukua hatua stahiki ikiwemo za kisheria inapobidi, Sote kwa nafasi zetu tuendelee kuihimiza jamii na kuwa mfano katika kutekeleza sheria tulizozitunga sisi wenyewe na kutunza mila, desturi na tamaduni zetu.”

Kwa upande mwingine, amezitaka Wizara za kisekta zisimamie kikamilifu sheria, kanuni na miongozo iliyopo pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaobainika kufanya vitendo kinyume cha sheria na maadili ya Taifa.

Amezitaka Asasi za Kiraia zitekeleze majukumu yao kwa mujibu wa vibali vyao vya usajili. “Kwa taasisi zitakazobainika kwenda kinyume na malengo ya usajili ikiwemo kuhamasisha mmomonyoko wa maadili na vitendo vinavyokinzana na mila, tamaduni na desturi zetu, zitachukuliwa hatua za kisheria.”

Matajiri wazuia usajili wa Bellingham Man Utd
Frank Lampard afichua kilichomrudisha Chelsea