Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji wa kiwanda cha nguo cha Compagnie Mauricienne De Textile Ltee kilichopo mjini Latour Koenig nchini Mauritius kuja kuwekeza Tanzania.

Majaliwa amesema hayo wakati alipotembelea kiwanda hicho kinachotumia teknolojia ya kisasa na chenye uwezo wa kutengeneza tani milioni 40 hadi 50 kwa mwaka, ambapo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao kuja nchini Tanzania na kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza nyuzi pamoja na nguo kwa kuwa kuna malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji huo.

“Tumefarijika na uwekezaji wenu na tumejionea namna ambavyo mnavyoendesha kiwanda chenu kuanzia utengenezaji wa nyuzi hadi nguo, hivyo tunahitaji viwanda kama hivi nchini Tanzania kwa sababu sisi tunazalisha pamba nvingi na yenye ubora unaokubalika kimataifa,” amesema Majaliwa.

 

Majaliwa amesema kuwa Tanzania inalima pamba nzuri, hivyo madhumuni  ya kuwakaribisha wawekezaji hao kuja Tanzania na kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza nyuzi yanalenga kuboresha kilimo cha pamba na kuwawezesha wakulima kupata tija.

“Hawalimi wananunua kutoka nje ya nchi yao, hivyo wakija kuwekeza Tanzania itawarahisishia kupata malighafi ya uhakika na kwa urahisi ”  amesema Majaliwa.

Aidha, Majaliwa ametoa wito kwa wananchi wenye uwezo kuhakikisha wanajenga viwanda vya nyuzi kwenye mikoa yote inayozalisha pamba ili waweze kuiongezea thamani kabla ya kuiuza.

Naye Mkurugenzi wa Fedha wa kiwanda hicho, David Too Sai Voon amesema wamefurahishwa na mualiko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya nyuzi na nguo.

Amesema kiwanda chao kilianzishwa mwaka 1986 na kwa sasa kimeajiri wafanyakazi 18,000 ambapo mauzo yao kwa ni dola milioni 200.

“Nguo tunazotengeza ni za kiwango cha kimataifa na tunauza katika maduka makubwa barani Ulaya,” – David Too Sai Voon

Majaliwa atembelea kiwanda cha nguo Mauritius, akaribisha wawekezaji kuja Tanzania
Amissi Tambwe, Donald Ngoma Kuikosa Azam FC