Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania kuna viwanda vitano vya sukari ambavyo ni Mtibwa, Mahonda (Zanzibar), TPC, Kilombero na Kagera vinavyozalisha tani 320,000 kwa mwaka huku mahitaji ni tani 420,000.

Majaliwa amesema hayo leo Machi 21, 2017 alipotembelea kiwanda cha sukari cha Kampuni ya Alteo ya Nchini Mauritius chenye uwezo wa kukamua tani 400 za miwa kwa saa na kuzalisha tani 170,000 za sukari kwa mwaka.

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akikagua shamba la miwa wakati alipotembelea kiwanda cha sukari cha Alitel nchini Mauritius Machi 21, 2017

Kampuni ya Alteo inamiliki kiwanda cha sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro  kwa ubia na Serikali ya Tanzania na  kinazalisha tani 110,000 kwa mwaka.

Majaliwa amefika kiwandani hapo kujionea namna wanavyozalisha sukari kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ambapo pia amefanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda hicho na kuwashawishi waongeze maeneo ya uwekezaji nchini.

“Tekonolojia wanayoitumia katika uendeshaji wa kiwanda chao ni nzuri hivyo tumewashawishi waje kuongeza maeneo ya uzalishaji wa sukari nchini ili tuweze kukidhi mahitaji,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mfumo wa kompyuta wa kiwanda cha sukari cha Alitel nchini Mauritius Machi 21, 2017.

Aidha, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed amesema Zanzibar kuna kiwanda kimoja cha sukari ambacho uzalishaji wake haukidhi mahitaji kutokana na uhaba wa malighafi.

Kufuatia hali hiyo, Dkt. Khalid ameikaribisha kampuni ya Alteo kwenda Zanzibar kushirikiana na Serikali katika uwekezaji hususani kwenye viwanda vya sukari.

Kwaupande wake Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Patrick de Labauve amesema wamekubali kuongeza maeneo ya uwekezani wa mashamba ya miwa nchini.

Pia ameomba Serikali iwapatie fursa ya uwekezaji katika sekta ya utalii mkoani Kilimanjaro. “ Kuna vivutio vingi vya utalii ukiwemo mlima Kilimanjaro,”.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda cha sukari cha Alitel nchini Mauritius Machi 21, 2017.

Kigwangalla ang'aka kuhusu mapenzi ya jinsia moja
Meya Dar kuhudhuria mkutano wa ICLEI Afrika Kusini