Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa atamuagiza Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha kwenda katika Kata ya Kiomoni kufanya tathmini ya ardhi ya wananchi ili kubaini thamani halisi ya maeneo hayo ili wananchi waweze kufidiwa.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya wananchi wa eneo hilo kutoa malalamiko kwa waziri Mkuu kuhusu kutoridhishwa na fidia ya maeneo yao yaliyochukuliwa na kampuni ya Neelkanth inayomiliki kiwanda hicho cha kuzalisha chokaa.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kiomoni katika mtaa wa Kiomoni wilayani Tanga akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.

Amesema kuwa atamtuma Mthamini Mkuu aende kubaini nani anadai nini na anamiliki nini ili atoe kibali cha ulipwaji ili muwekezaji aweze kupewa kibali cha kuwalipa fidia yao.

”Tunataka jambo hili liishe kabla ya mwishoni mwa mwaka huu kila kitu kiwe kimekamilika na hakuna mwananchi hata mmoja atakayepoteza haki yake ya msingi.”amesema Majaliwa

Aidha, ameongeza kuwa uwekezaji huo ni muhimu kwa kuwa ni sehemu ambayo viwanda mbalimbali vya saruji nchini vinategemea kwa kupata malighafi, hivyo alimpongeza muwekezaji na kumshauri aongeze uzalishaji kadiri anavyoweza.

Pia, ameongeza kuwa wawekezaji katika sekta ya viwanda ni muhimu kwa sababu wanaunga mkono mkakati wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kukuza uchumi kutoka wa chini hadi wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda.

 

Real Madrid waombwa kusahau yaliyopita
Alex Sandro awanyima usingizi Man Utd, Pogba ahusishwa