Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wapya wa Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU)wajipime kama wako tayari kuwatumikia wananchi na kama sivyo waachie ngazi.
Majaliwa ametoa onyo hilo wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Mwangongo na vijiji vya jirani mara baada ya kukagua soko la pamba kwenye kijiji hicho, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo, aliwataka wajumbe hao wajitafakari upya na kujihoji kama wameomba vyeo hivyo kwa ajili ya kupata utajiri ama kuwatumikia wananchi.
“Napenda kusisitiza kwamba ule mfumo wa zamani wa ushirika hivi sasa haupo. Kama uliomba cheo hicho kwa ajili ya kupata utajiri, ni bora ujiondoe sasa hivi, njoo uniambie wakati bado niko kwenye ziara ya mkoa huu, tutatafuta wajumbe wengine ambao ni waaminifu,” alisema.
Amesema tofauti na ilivyokuwa awali, Serikali ya awamu ya tano inataka kuona ushirika wa sasa ukirejesha matumaini kwa wananchi.
Majaliwa amesema zamani, ushirika ulimwezesha mwananchi kununua baiskeli au redio lakini kutokana na hali ilivyobadilika, jambo hilo lilikuwa haliwezekani. “Tunataka ushirika wa sasa ubadilike na umwezeshe mwananchi kununua gari la kutembelea ama kujenga nyumba bora,” amesema.
Aidha, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa alisema barabara ya kutoka Kolandoto hadi Igelekelo imeshafanyiwa usanifu na kwamba Serikali ya Ujerumani imeanza mazungumzo na Serikali ya Tanzania kuhusu ujenzi wake.
“Kazi ya usanifu wa barabara hiyo imekamilika, tumeanza mazungumzo ya kutafuta wafadhili. Ujenzi wake ukikamilika, utakuwa umerahisisha kuunganisha mkoa huu na mikoa ya Singida, Arusha na Manyara.”
“Kutoka Shinyanga hadi Singida tutakuwa tumepunguza km. 250, wakati kutoka Shinyanga jadi Karatu tutakuwa tumepunguza km. 400 badala ya kupita kwanza Nzega, uende Singida hadi Karatu,” alisema.
Waziri Mkuu bado anaendelea na ziara yake Wilayani Shinyanga ambapo leo atakagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.