Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewasihi Watanzania wanaofanya kazi katika viwanda mbalimbali nchini kufanya kazi kwa bidii na kuwa waaminifu.

Majaliwa amesema hayo leo Julai 30, 2017 wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha gesi cha Ikama kilichoko wilayani Rungwe, amesema Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda hivyo ni vema watakaopata fursa ya ajira katika viwanda hivyo kuwa waadilifu.

Amesema wakati Serikali ikiendelea kuwakaribisha wawekezaji nchini, wananchi walioajiriwa kwenye maeneo hayo wawe waaminifu. “Mnatakiwa muwe waaminifu, msibebe kitu chochote ndani ya kiwanda bila ya ridhaa ya wamiliki kwa kuwa mtaonyesha taswira mbaya kwa wawekezaji.”

Amesema uaminifu wao ndio utawezesha Watanzania wengi kupata ajira kwenye viwanda hivyo ambavyo vimejengwa  katika maeneo yao.

Kabla, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na kampuni ya TOL Gases, Mhandisi Harold Temu alisema kiwanda kinauwezo wa kuzalisha tani 46 kwa siku.

Alisema gesi inayozalishwa kiwandani hapo ni ya Carbon Dioxide ambayo inauzwa nchini na nchi jirani za Zambia, Malawi, Zimbabwe na Congo.

Mhandisi Temu alisema wateja wakubwa wa gesi hiyo ni viwanda vya kutengenezea soda, bia na pia hutumika katika kuhifadhia chakula na kwenye vifaa vya kuzimia moto.

Mapema Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kuchakata majani ya chai cha Katumba, ambapo alisema Serikali inaimarisha Ushirika wa zao hili ili wakulima waweze kupata tija.

Video: Simba kwachafuka, Wazee Simba wagomea mabadiliko
Makamu wa Rais Kenya azungumzia tukio la uvamizi nyumbani kwake