Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda, hivyo amewakaribisha wawekezaji kutoa Iran ili kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na uvuvi.
Majaliwa amesema hayo leo Machi 17, 2017 alipokutana na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mousa Farhang kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa Serikali imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake, hivyo wanahitaji uwekezaji mkubwa kwenye sekta mbalimbali.
“Tumedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kutoa Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na uvuvi,” amesema.
Majaliwa pia amewakaribisha raia wa Iran kuitembelea Tanzania kama watalii kwa sababu kuna fursa nyingi za utalii ukiwemo mlima wa Kilimanjaro ambao unaongoza kwa urefu barani Afrika pamoja na mbuga nyingi zilizosheheni wanyama.
Aidha, Balozi Farhang ameipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi. Amesema Tanzania ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine barani Afrika.
Amesema kuwa ufisadi na dawa za kulevya ni tatizo kubwa ambalo linazikabili nchi nyingi, hivyo kitendo cha Serikali ya Tanzania kupambana na tatizo hilo ni cha kupongezwa na kitaiwezesha kusonga mbele kiuchumi.
Pia ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri na Iran ambao umedumu kwa miaka 40, hivyo ameiomba ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo, ambapo Waziri Mkuu amekubali.
“Tanzania na Iran wana uhusiano wa kihistoria ambao unadhihirishwa na uwepo wa Washirazi wengi husan visiwani Zanzibar ambao wanaasili ya Iran na maeneo ya kusini mwa Iran kuna Watanzania wengi hata muonekano wao ni wa Kitanzania,” amesema.