Wawekezaji waliobobea kwenye sekta ya mbolea wamekaribishwa ili kuja kufungua viwanda vya mbolea nchini kutokana na uwepo wa changamoto ya hitaji hilo na kwamba Tanzania ina rasilimali ya gesi ambayo inaweza kutumika kutengeneza mbolea.
Mwaliko huo umetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akizungumza kwenye mjadala uliohusu Uimarishaji wa Soko la Mbolea kama njia ya kuondoa njaa barani Afrika uliofanyika jijini St. Petersburg, Urusi huku akisema uamuzi wa Rais Dkt. Samia wa kuongeza bajeti ya kilimo una nia ya kuifanya Tanzania iwe eneo la uzalishaji la kulisha Afrika Mashariki, SADC na Afrika.
Amesema, “bado tuna changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa sababu ikikosekana inaathiri uzalishaji wa chakula, Mbolea kwa sasa ndiyo msingi wa uzalishaji chakula, tunatumia fursa hii kutafuta marafiki ambao wako tayari kuja kuwekeza kwenye mbolea. Mahitaji yetu ni zaidi ya tani 800,000 wakati uzalishaji wetu ni tani 200,000.”
“Tukifanikiwa kuongeza uzalishaji wa mbolea, tutakuwa na nafasi ya kuzalisha chakula zaidi. Jukwaa hili ni nafasi pekee ya kualika wawekezaji waliobobea kwenye maeneo kama haya, uzalishaji wetu unatumia zaidi ya asilimia 80 na kwa maana hiyo tunalazimika kutumia fedha nyingi ili kuagiza mbolea kutoka nje na msisitizo wa sasa ni kuzalisha mbolea yetu,” amesema Majaliwa.